Katika hatua za mwanzo za ushirikiano huu, Kampuni ya Tigo Tanzania itachagua maduka matatu ambayo Kupatana.Com itayatumia kuwawezesha wateja wa Tigo kuuza simu zao zilizotumika kwa kupitia jukwaa la Kupatana.com.
Akizungumza wakati wa kusaini makubaliano baina ya pande hizo mbili jijini Dar es Salaam, Meneja wa Miradi wa Kampuni ya Tigo, Anthony Njau alisema, “tukiwa ni kampuni ya mtindo wa maisha ya kidijitali, tumeona kwamba hivi sasa Watanzania wamehamasika mno katika kufanya biashara kupitia njia ya mtandao.”Njau aliongeza kwamba , “Mtandao na wavuti wa Kupatana.com unatoa jukwaa zuri ambalo linabadilisha namna ambavyo watu wanaishi kwa kuwezesha kupatikana kwa huduma na bidhaa katika njia sahihi na rahisi.”
“Lengo la muda mrefu ni kuwapatia wateja wetu jukwaa ambalo wanaweza kupakua vifaa ambavyo vilishatumika ili kuviboresha na kwa upande wa Tigo kuuza vifaa vipya, kuongeza usambazaji na kuwa na mafanikio katika jaribio hili la msingi, Tigo na Kupatana.com zitapanua wigo wa huduma hii na kuhakikisha inapatikana kwa urahisi katika maduka yote 52 ya Tigo ambayo yamesambaa kote nchini,” alisema Njau.
Mkurugenzi wa Kupatana.com, Philip Ebbersten, alisema kwamba kupitia matumizi ya jukwaa hilo, wauzaji (kampuni na watu binafsi) wataweza kuwafikia maelfu ya wanunuzi muhimu kila siku bila kujali maeneo yao ya kijiografia.
Alifafanua kuwa kuorodhesha bidhaa katika jukwaa hilo ni bure na kuwashauru wateja umuhimu wa kufuata kanuni na miongozo salama kwa bidhaa zote zitakazotangazwa Kupatana.com ili waweze kuzitapa kwa usalama na uelewa zaidi.