Tigo kwa mara nyingine mdhamini rasmi wa mawasiliano kwenye maonyesho ya Sabasaba 2019
- Wateja wake kupata ofa maalum kwenye data na simu janja msimu huu wa Sabasaba
Dar es Salaam, Juni 29, 2019. Kampuni ya simu za mkononi ya Tigo kwa mara ya nne mfululizo imekuwa mdhamini rasmi wa mawasiliano kwenye maonyesho ya 43 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam maarufu kama Sabasaba ambayo huandaliwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade).
Maonyesho ya Sabasaba yataanza tarehe 28 mwezi Juni hadi tarehe 8 mwezi Julai, yakiwa na kauli mbiu ‘Usindikaji wa Mazao ya Kilimo kwa Maendeleo Endelevu’
Akizungumzia udhamini huo, Meneja Mawasiliano wa Tigo Woinde Shisael alisema, Tigo imekuwa ikidhamini maonyesho hayo kwa miaka minne mfululizo kwenye eneo la mawasiliano na kuongeza kuwa udhamini huo pia unalenga kuunga mkono jitihada za serikali za kukuza biashara na kukuza viwanda vya ndani kwa ajili ya ukuwaji wa uchumi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano kwa Umma na Mawasiliano wa TanTrade Theresia Chilambo aliishukuru kampuni ya Tigo kwa kudhamini maonyesho hayo kwa mara ya nne.
Theresia alisema, TanTrade inayo furaha kuwa na mshirika wa kuaminika kwenye sekta ya mawasiliano na kuongeza kuwa mamlaka hiyo inasubiria kwa hamu ushiriki wa Tigo katika maonyesho hayo ya kimataifa.
Pamoja na udhamini huo, Tigo pia imeungana na makampuni sita ya kutengeneza simu kutoa ofa za kipekee kwa data pamoja na simu janja kwa maelfu ya wateja wao wataokuwa wanashiriki maonyesho hayo jijini Dar es Salaam.
“Wakati tunaingia msimu mwingine wa kusisimua wa Sabasaba, tumeaanda ofa nzuri za data pamoja na simu janja kwa ajili ya wateja wetu. Tunashirikiana na Infinix, Itel, Nokia, Samsung, TECNO Mobile na KaiOS kuwapa wateja wetu siyo tu chaguo pana la huduma mbali mbali bali pia aina mbali mbali za simu janja na data ambavyo vinakidhi mahitaji yao,” alisema Woinde
Aliongeza “Wateja wetu wataweza kupata ofa za kuvutia ikiwa ni pamoja na simu janja za gharama nafuu ambazo zitapatikana kwa kuanzia Tshs 74,900 zikiwa na GB 96 za intaneti zinazoweza kutumika kwa kipindi cha mwaka mmoja. Tigo pia itakuwa na promosheni maalum kwa ajili ya wateja wa Tigo Pesa pamoja na wateja watakaosajili laini zao kwa utaratibu mpya wa alama za vidole,”
Akifafanua zaidi Woinde alisema, wateja wapya wa Tigo Pesa kipindi cha Sabasaba wataweza kutuma pesa (Tigo kwenda Tigo) pasipo makato kwa kipindi cha miezi 3 na kuongeza kuwa mteja atakayejisajili kwa kutumia utaratibu mpya wa alama za vidole atazawadiwa dakika 100 za bure kutoka Tigo.
Kwa mujibu wa Woinde, Tigo imejiandaa kikamilifu kutoa ofa mbali mbali ikiwamo data, simu janja, huduma za kifedha pamoja na huduma kwa ajili ya biashara ndogo, kubwa na za kati ikiwa ni jitihada za kuhamasisha maisha ya kidijitali ambayo yataongeza matumizi ya simu janja na matumizi ya data pamoja na mtandao wenye kasi wa 4G.
“Napenda kuwakaribisha wateja wote wanaoishi Dar es Salaam na watakaotoka nje ya Dar es Salaam kutembelea banda la Tigo katika msimu huu wa Sabasba ili waweze kujipatia huduma na bidhaa bora pamoja na ofa mbali mbali kutoka mtandao unaoongoza wa Tigo,” alisema Woinde.
Banda lililonakshiwa vyema la Tigo litakuwa na sehemu ya wateja kuona na kujaribu vifaa mbali mbali ikiwemo simu, dawati kwa ajili ya kuhudumia wateja ambao ni biashara, sehemu za burudani huku likitarajia kuvutia watembeleaji 500 kwa siku.