Hatua hiyo itasaidia kuboresha zaidi huduma na kukuza sekta ya mawasiliano nchini.
Dar es Salaam. Novemba 4, 2019. Kampuni ya Mawasiliano ya MIC Tanzania Public Limited Company (Tigo), leo imetangaza rasmi kuungana na kampuni ya Zanzibar Telecom Public Limited Company (Zantel) baada ya kukamilika kwa taratibu zote za kisheria na kiumiliki ambapo lengo kuu ni kukuza na kuboresha huduma za mawasiliano nchini.
Pamoja na kupata vibali kutoka mamlaka zinazohusika, mchakato wa kuhamisha hisa na umiliki kamili kutoka Zantel kwenda Tigo sasa umekwisha kamilika. Kufuatia kukamilika kwa zoezi hili sasa makampuni haya yataunganisha shughuli zake za kiutendaji Tanzania Bara na Visiwani Zanzibar.
Akizungumza kuhusu muungano huo, Mkurugenzi Mkuu wa Tigo, Simon Karikari alisema hatua hiyo ina manufaa makubwa kwa Taifa; “Ninaamini kuwa kuunganishwa kwa kampuni hizi - Tigo na Zantel kutajenga huduma jumuishi kwa watanzania wote siku za usoni. Wateja wote wa Tigo na Zantel wataweza kufurahia huduma bora kutoka kwenye soko imara litakalosaidia kuchochea ubunifu kwenye sekta ya mawasiliano,” alisema Karikari.
Muunganiko wa makampuni haya mawili utasaidia katika kuimarisha utoaji wa huduma kwa wateja wa Tigo na Zantel waliopo kote Tanzania Bara na Visiwani. Aidha, muungano huu utawezesha kupanua wigo wa huduma zetu pamoja na kuongeza ubora wa upatikanaji wa mawasiliano katika maeneo ya mijini na vijijini. Vile vile muungano huu utasaidia katika usambazaji wa huduma za mawasiliano kwa makampuni na taasisi mbalimbali nchini na pia kupanua huduma za kifedha kwa njia ya simu za mkononi.
Tunategemea mafanikio chanya kutokana na muunganiko wa makampuni haya mawili wenye lengo la kuchangia kwenye maendeleo ya Taifa.
Zoezi la kuunganisha taratibu za kiutendaji wa makampuni haya mawili zinatazamiwa kuanza hivi punde. Aidha, wateja wa Tigo na Zantel wataendelea kupata huduma bila usumbufu wowote kutoka mtandao husika kwani namba na laini za wateja hazitabadilika.
**Mwisho**
Factsheet:
Zantel na Tigo Pamoja
Jumla ya Wateja: 12,883,000
Jumla ya Wateja wa Huduma za kifedha kwa njia ya simu za mkononi: 7,350,000
Kwanini kampuni ya Tigo na Zantel zinaungana?
Kwa sasa soko la mawasiliano Tanzania limegawanyika sana hivyo kulikuwa na uhitaji wa kuunganisha makampuni haya. Kuunganishwa kwa shughuli za kiutendaji baina ya Tigo na Zantel kutaweka mazingira shindani na yenye tija kwa taifa, kutachochea maendeleo na ubunifu katika sekta ya mawasiliano na zaidi kuimarisha uwezo wa makampuni haya ili kuyawezesha kutoa huduma zenye ubora wa kimataifa kwa wateja wao waliopo Tanzania Bara na Visiwani.
Nini manufaa ya muunganiko huu kwa wateja, sekta ya mawasiliano na Taifa kwa ujumla.
- Sekta ya mawasiliano: Kukuza na kuimarisha sekta, kuongeza uwekezaji na kuboresha huduma pamoja na kuchochea ubunifu
- Kwa Taifa: kuchangia katika maendeleo ya Taifa kwa ujumla na katika sekta ya mawasiliano ya simu.
- Kwa Wateja: Utaleta manufaa makubwa zaidi kwa wateja na biashara kwa ujumla kwa kuyafanya makampuni haya kupanua wigo wa uwekezaji na kuwapa wateja huduma bora zaidi, kuboresha upatikanaji wa mtandao na kukuza ubunifu na teknolojia.
Kutopatikana kwa huduma za mawasiliano wakati wa zoezi la kuunganisha shughuli za kiutendaji;
Wateja wataendelea kufurahia huduma zote bila matatizo kutoka mtandao husika yaani Zantel au Tigo. Laini za simu na taarifa za wateja hazitabadilika na hakutakuwa na usumbufu katika upatikanaji wa mawasiliano na huduma nyingine.
Athari kwa Wafanyakazi
Kwa sasa, Tigo na Zantel zitaendelea kujiendesha kama kampuni tofauti na biashara zitaendelea kama kawaida. Wakati zoezi la kuunganisha makampuni haya mawili likiendelea, kutakuwa na uhamishaji wa rasilimali ndani ya Tigo na Zantel ambao hautaathiri shughuli za kiutendaji na tunategemea kutakuwa na athari ndogo tu kwa rasilimali watu (wafanyakazi) wa makampuni haya mawili.
Nini kinafuata?
Tunaendelea kuendesha biashara kama ilivyo ada na kwa sasa kila kampuni itafanya kazi zake kama taasisi inayojitegemea. Hata hivyo katika wiki zijazo zoezi la uunganishwaji wa shughuli za kiutendaji za makampuni haya utaanza na tutaendelea kutoa taarifa kwa wanahabari kuhusu hatua muhimu zitakazofikiwa wakati wa zoezi hili.