Kupitia promosheni hiyo, wakala aliyefanya vizuri kuliko wote nchini, amepokea zawadi ya fedha taslimu shilingi milioni 20 wakati mawakala wengine wanaofuatia kwa kufanya vizuri kutoka kanda nne wakipokea jumla ya shilingi milioni 40.
Akiongea wakati wa hafla fupi ya kuwakabidhi washindi zawadi zao, Mkuu wa Huduma za Kifedha wa Tigo Hussein Sayed alisema promosheni hiyo imewekwa maalum kwa ajili ya kuwashukuru na kuwazadia mawakala wanaofanya vizuri katika kipindi cha mwisho wa mwaka.
Hussein alisema, washindi 20 kutoka kanda nne ambazo ni Pwani, Kusini, Kaskazini na Kanda ya Ziwa walipatikana ambapo kila kanda ilitoa washindi watano ambao kila mmoja alijinyakulia zawadi ya fedha taslimu shilingi milioni mbili wakati mshindi wa jumla akiondoka na shilingi milioni 20.
“Jumla ya mawakala 90,000 walishiriki katika promosheni hii ya nchi zima iliyoanza tarehe 1 Disemba na kumalizika tarehe 31 Disemba 2018,” alisema
Kwa upande wake Mkuu wa Bidhaa Huduma za Kifedha kwa njia ya Simu, James Sumari aliongeza kwa kuwashukuru Mawakala kwa mchango wao mkubwa katika kufikisha huduma za kifedha kwa wantanzania
“Tunayofuraha kutoa mchango unaowezesha wananchi wengi kufikiwa na huduma za kifedha. Kupitia huduma ya Tigo Pesa, tumewawezesha mamilioni ya Watanzania kutuma na kupokea fedha na kufanya malipo mbali mbali kwa urahisi na kwa usalama. Tigo Pesa ni zaidi ya suluhisho kwa malipo na huduma rahisi za kifedha, ni sehemu ya maisha,” alisema Sumari.
Vicky Ibrahim ambaye ni mshindi mkubwa katika promosheni hiyo kutoka Kanda ya Pwani mkoa wa Dar es Salaam alisema, shilingi milioni 20 alizojishindia zitamsaidia kupanua biashara yake hiyo ya Tigo Pesa huku akiishukuru kampuni ya Tigo kwa zawadi hiyo.
“Ninayo furaha kubwa kupokea zawadi hii ambayo kimsingi sikuitarajia. Nitatumia fedha hizi kupanua biashara yangu na kutatua matatizo yangu binafsi ambayo yanahitaji fedha,” alisema
Tigo Pesa inashikilia nafasi ya pili hapa nchini kama mtoa huduma za kifedha mkubwa kwa njia ya simu. Tigo Pesa pia imefungua milango ya ugunduzi wa kidijitali Afrika Mashariki ikiwa ni kampuni ya kwanza kuanzisha huduma ya kutuma fedha kwa njia ya simu kwa nchi nyingine, kutuma pesa kwenda mitandao mingine na kuingia kwenye pochi moja, huduma ya jihudumie mwenyewe pamoja na App ya kisasa ya Tigo Pesa inayorahisha sana kufanya miamala.