Dar es Salaam, 14 Machi, 2018. Kampuni inayoongoza kwa huduma za fedha kwa njia ya mtandao, Tigo Tanzania kupitia huduma yake ya Tigo Pesa leo imewazawadia wakala wake mamilioni ya pesa kwa utendaji wao mzuri.
Wakala RBB RBB ya Sinza, Dar es Salaam ilijishindia TZS 10 millioni kutoka Tigo Pesa, huku Said Khatib wa Mkunazini, Zanzibar akijinyakulia zawadi ya pili ya TZS 5 millioni katika promosheni iliyohusisha mawakala zaidi ya 73,000 wa Tigo. ‘Nilishinda zawadi ya kanda katika promosheni iliyofanyika mwezi Desemba kwa hiyo nafurahi kuwa uwekezaji na juhudi nilizofanya katika kipindi hiki vimeniwezesha kutangazwa kama mojawapo wa washindi wa kitaifa,’ Khatib alisema.
Pamoja na zawadi hizio kwa washindi wa kitaifa, Tigo pia ilitoa zawadi nane za TSH 3 millioni na TZS 2 millioni kwa mawakala bora kutoka kila kanda nchini. Pia zawadi za bonasi zilitolewa kwa mawakala wote waliofikia malengo waliowekewa katika kipindi cha promosheni hiyo.
Mojelwa Mlinga wa Ukonga, Dar es Salaam aliyeibuka kama wakala bora wa kanda ya Pwani na kujinyakulia kitita cha TZS 3 milioni alisema kuwa atatumia hela alizoshinda kuboresha mtaji wake wa biashara. ‘Nilishinda zawadi ya pili kitaifa katika promosheni iliyofanyika mwezi Desemba na nilikuwa natarajia kushinda zawadi ya kwanza kitaifa, ila nashukuru kuwa nimefanikiwa kupata zawadi ya kanda,’ alisema.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi zawadi kwa washindi iliyofanyika katika ofisi za Tigo jijini Dar es Salaam, Afisa Mkuu wa Huduma za Kifedha wa Tigo, Hussein Sayed alisema kuwa lengo kuu la promosheni hiyo ilikuwa ni kuwadhamini na kuwashukuru mawakala zaidi ya 73,000 wa Tigo Pesa walioshiriki katika promosheni hiyo kote nchini.
“Ningependa kuwapongeza mawakala wetu kwa kazi kubw wanayofanya ya kuhakikisha kuwa huduma za kifedha zinapatikana kwa urahisi kwa watu wote kote nchini,’ alisema.
Tigo Pesa ni huduma ya fedha ya simu za mkononi ya pili kwa ukubwa nchini.
Kampuni ya Tigo ilianza kutoa huduma nchini Tanzania mwaka 1995 na kwa miaka mitatu mfululizo ndiyo kampuni ya simu inayokua kwa kasi zaidi nchini. Kwa sasa Tigo ndio kampuni ya simu za mkononi ya pili kwa ukubwa nchini inayohudumia wateja zaidi ya 11.6 milioni.
Tigo ni kampuni inayoongoza kwa mageuzi ya kidigitali nchini na inatoa huduma bora za kipekee za sauti, SMS na intaneti ya kasi ya juu ya 4G inayopatikana katika miji 24 nchini kote. Tigo pia inafahamika kwa promosheni kabambe na ofa bunifu kwa wateja wake.