Hii ni mara ya nane kwa Tigo kutoa malipo ya robo mwaka kwa watumiaji wake wa huduma ya Tigo Pesa jambo ambalo limeifanya kuwa kampuni ya kwanza ya simu duniani kuanzisha utaratibu wa malipo ya aina hiyo tangu Julai 2014.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na kampuni hiyo leo inaonesha malipo ya robo mwaka unaomalizika mwishoni mwa Machi 2016 umekua kwa asilimia 18ukilinganisha na robo mwaka iliyomalizika Desemba 2015 ambapo malipo kwa wateja yalikuwa 4.4bn/-.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Tigo wa Huduma za Fedha kwa Njia ya Mtandao Ruan Swanepoel watumiaji wa Tigo Pesa wameshapata malipo ya jumla ya 40.7bn/- tangu kuanzishwa kwa zoezi hili. Malipo hayo inayolipwa kama riba kutokana na amana za watumiaji wa Tigo Pesa ambazo huwekezwa na Tigo katika mabenki mbalimbali humu nchini.
“Wanaonufaika na malipo haya ni pamoja na wateja binafsi, mawakala wa rejareja pamoja na wadau wengine wa kibiashara wa Tigo Pesa ambapo kila mmoja anapokea malipo kulingana na thamani ya fedha ya kielektroniki waliyoiweka katika pochi zao za Tigo Pesa,” alisema Raun.
Raun aliongeza, “Tunayo furaha kutangaza ongezeko la malipo kwa wateja wetu kwa mara ya nane mfululizo. Hii inaonesha kujituma kwetu kutoa huduma ya fedha kwa wateja wetu na nchi kwa jumla kupitia huduma za Tigo Pesa.
Alibainisha kuwa kuongezeka kwa faida kwa Tigo kunatokana kuimarika kwa soko la huduma ya Tigo Pesa sambamba na kuongezeka kwa idadi ya watumiaji wa huduma hiyo. Tigo Pesa hivi sasa ina mtandao mkubwa wa mawakala wapatao 50,000 wanaopatikana nchini kote.
Kama ilivyokuwa awali, kwa mujibu wa Swanepoel, malipo wanayopata wateja yanakokotolewa kwa kuzingatia wastani wa salio analokuwa nalo mteja katika akaunti yake ya kila siku ndani ya pochi ya simu na kuongeza kuwa utaratibu wa kugawa upo kwenye taratibu zilizotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Februari 2014.